Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amelitaka Shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania (TFC) kushirikiana kikamilifu na Chama Kikuu cha Ushirika Njombe (NJORECU) na kuhakikisha mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea unaanza kabla ya mwezi Juni mwakani. Waziri Hasunga amesema hayo wakati akizungumza na Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Njombe, Mjumbe kutoka Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) pamoja na muungano wa makampuni ya uwekezaji kutoka China jijini Dar es salaam.
Waziri huyo amesema kuwa, baada ya ujenzi wa kiwanda hicho kukamilika. wanaushirika wa chama hicho cha NJORECU na wakulima wote nchini watanufaika kwani kitaongeza urahisi wa upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu kutokana na uzalishaji kufanyika hapa nchini. Waziri Hasunga ameshauri kuandaa andiko la mradi huo litakaloeleza aina ya mbolea itakayozalishwa na taarifa zote zinazohitajika katika kufanikisha mradi huo.
Wawekezaji hao kutoka China kwa kushirikiana na NJORECU wamejipanga kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea pamoja na kiwanda cha kufungasha viuatilifu vinavyotumika katika kilimo. Katika kikao hicho, imeelezwa kuwa wawekezaji hao wapo tayari kuchangia asilimia 40% na NJORECU asilimia 60%.