Home BENKI BoT: hatuna utaratibu wa mawakala uombaji leseni

BoT: hatuna utaratibu wa mawakala uombaji leseni

0 comment 262 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema haina utaratibu wa kuwataka waombaji wa leseni au usajili wowote kutumia washauri kwenye uandaaji na uwasilishaji wa maombi ya leseni.

Taarifa ya BoT imesema imebaini uwepo wa taasisi, kampuni na watu binafsi wanaojitangaza kuwa mawakala au washauri elekezi (consultant).

“Tumebaini kuwa baadhi ya matangazo yanayotolewa na washauri sio sahihi hasa gharama zinazohusika,.

Tunapenda kuutaarifu umma kuwa hatuna utaratibu wa kuwataka waombaji kutumia washauri,” imesema taarifa ya BoT.

Taarifa hiyo inabaininsha kuwa, watu hao wanaotoa huduma ya kusaidia waombaji kupata leseni au usajili wa watoa huduma ndogo za fedha, maduka ya kubadilishia fedha za kigeni, benki na taasisi za fedha, watoa huduma na mifumo ya malipo pamoja na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zinazosimamiwa na BoT.

Aidha, BoT imewataka washauri hao kutenganisha gharama za huduma za ushauri na zile za leseni za Benki Kuu kwenye matangazo yao.

“Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Sheria ya Huduma ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 na kanuni zake zimeainisha viwango vya mitaji na gharama za maombi ya leseni ya kila aina ya taasisi,” inaeleza BoT.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba ada ya maombi ya leseni kwa upande wa Benki na Taasisi za Fedha ni Sh milioni kumi (10,000,000) na hakuna ada ya leseni.

Kwa upande wa maduka ya kubadili fedha za kigeni ada ya maombi ya leseni ni Sh milioni moja (1,000,000) na ada ya leseni ni Sh laki tano (500,000) kwa mwaka kwa kila tawi.

Watoa huduma ndogo za fedha (mtu binafsi) watatakiwa kulipa Sh laki tatu (300,000) ada ya maombi ya leseni na hakuna ada ya leseni.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa watoa huduma ndogo za fedha (Kampuni) watalipa ada ya maombi ya leseni Sh laki tano (500,000) na hakuna ada ya leseni huku watoa huduma za mifumo ya malipo watalipa ada ya maombi ya leseni Sh milioni moja (1,000,000) na milioni kumi na mbili (12,000,000) ikiwa ni ada ya leseni kwa miaka mitano.

Milioni moja (1,000,000) italipwa kama ada ya maombi ya leseni kwa watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu na milioni mbili (2,000,000) ikiwa ada ya leseni kwa kipindi cha miaka mitano.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter