Home VIWANDAUZALISHAJI Mradi wa Tsh milioni 50 wakabidhiwa Jumuiya Hifadhi ya Wanyamapori

Mradi wa Tsh milioni 50 wakabidhiwa Jumuiya Hifadhi ya Wanyamapori

0 comment 30 views

Mradi wa Tsh milioni 50 wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori (IWT) umekabidhiwa kwa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WAGA).

Mradi huo uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, umekabidhi mizinga ya kisasa 300, vifaa mbalimbali vya kufugia nyuki na kusindika asali vyenye gharama ya shilingi milioni 50.

“Endapo WAGA watashiriki na kutumia vyema mafunzo yatakayotolewa na wataalamu, mizinga hiyo itaweza kuzalisha asali wastani wa tani 10 zitakazokuwa na thamani ya shilingi milioni 150 kwa mwaka,” amesema Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana 10, 2024 katika hafla ya makabidhiano ya mizinga hiyo iliyofanyika Wilaya ya Mafinga, Mkoani Iringa.

Ametoa rai kwa Jumuiya ya WAGA kutunza na kutumia ipasavyo mizinga na vifaa hivyo viweze kuleta matokeo chanya.

Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Chana amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inakuja na mpango wa kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki unaohusisha programu maalum ya kuwezesha vijana na wanawake kuzalisha na kufanya biashara ya mazao ya nyuki.

“Mpango huu utachangia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 32,000 hadi kufikia tani 185,379 kwa mwaka, kuongeza kiwango cha asali kinachouzwa nje ya nchi kutoka asilimia 5 hadi 30, kuongeza fedha za kigeni kutoka dola milioni 8 hadi dola milioni 20 kwa mwaka” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu,Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkuruganzi wa Misitu na Nyuki, Deusdedit Bwoyo amesema kuwa makabidhiano ya mizinga hiyo ni sehemu ya mpango wa kuwezesha jamii zinazozunguka hifadhi kwenye mfumo wa ikolojia ya Ruaha – Rungwa kujikimu ili kupunguza utegemezi wa maliasili.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mradi utawezesha miradi yenye thamani ya shilingi milioni 337 kwa vikundi 21 vya ufugaji nyuki na kilimo katika Wilaya za Itigi, Mbarali na Mufindi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wadau wa Sekta ya Nyuki pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter