Home VIWANDA Uchafu wa mazingira waponza wamiliki wa viwanda Mikocheni

Uchafu wa mazingira waponza wamiliki wa viwanda Mikocheni

0 comment 134 views

Wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda katika eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam wamepewa mwezi mmoja kutatua kero ya uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo kwa kuzuia utiririshaji ovyo wa maji taka katika makazi ya watu, hali inayohatarisha afya za wakazi hao.

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Kangi Lugola alipotembelea viwanda vya Iron and Steel na MMI Intergrated Mills vilivyopo Mikocheni “B” jijini Dar es salaam ili kujionea hali halisi ya mazingira ya wakazi wa eneo hilo ambapo alitoa onyo kwa wale watakaokiuka agizo hilo kuwa, watachukuliwa hatua za kisheria.

Lugola ameagiza wamiliki wa viwanda hivyo kuyatibu maji machafu na kuhakikisha moshi wa viwanda hivyo hauleti madhara kwa wananchi, huku akiagiza kupelekewa taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo ndani ya mwezi mmoja.

Aidha amewakumbusha wamiliki wa viwanda mbalimbali nchini na wale wanaohitaji kuwekeza katika sekata hiyo  kuwa kabla ya kufanya hivyo ni vizuri wakaangalia namna ya kudhibiti athari mbalimbali zinazoweza kutokea.

Kwa upande wake, Mratibu wa NEMC Kanda ya Mashariki Japhary Chimgege amesema wamekuwa wakichukua hatua  mbalimbali kushughulikia usafi wa mazingira katika maeneo hayo kutokana na viwanda kuwa vingi. Chimgege ameongeza kuwa wamekuwa wakifuatilia wamiliki wa viwanda na kujiridhisha kuwa wanatekeleza sheria ya mazingira ili kulinda afya za wananchi waishio jirani na viwanda hivyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter