Biashara na teknolojia ni mambo ambayo yanaenda sambamba katika maendeleo. Kabla ya uelewa wa matumizi ya intaneti kwa manufaa ya biashara, wafanyabiashara walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta soko na kujitangaza ili waweze kupata wateja lakini tangu uelewa huu uanze kutumika, imekuwa rahisi kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao na kujitafutia wateja kwa muda mfupi.
Mitandao ya kijamii ikitumika vizuri kwa manufaa ya kujipatia kipato,mtu huona mahali hapo ni kama soko au ofisi ambapo unaweka bidhaa zako hadharani na kuvutia wateja kutoka kila kona ya nchi. Ni njia rahisi ya kujiingizia kipato, kujielimisha zaidi kibiashara, kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wengine na kukuza biashara yote. Yote haya katika kiganja cha mkono wako na kwa kutumia muda mfupi na gharama nafuu.
Wafanyabiashara wakitumia mitandao hii vizuri wanajihakikishia soko la uhakika kwani wanaweza kuongea na wateja wao mara kwa mara na hivyo kushauriana juu ya huduma na ubora wa bidhaa. Pia mfanyabiashara anaokoa gharama za kufanya matangazo kwani badala ya kulipa magazeti, redio au mabango, anaweza kufungua akaunti itayoeleza biashara kwa undani hivyo anakuwa anajitangaza mwenyewe bila gharama yoyote.
Kwa kutumia mitandao ya kijamii pia, mfanyabiashara anaweza kuwa chanzo cha ajira kwa mtu mwingine. Ili kuhakikisha wateja wako wanapata huduma bora zaidi na katika muda husika, biashara nyingi za mitandaoni huitaji madereva kwa ajili ya kufikisha bidhaa kwa wateja, mawakala ikitokea biashara imepanua wigo lake hadi kufikia mikoa mingine na ajira nyingine mbalimbali. Hivyo kwa kutumia mitandao kibiashara, ajira nyingi zaidi zinazaliwa.
Tanzania inakadiriwa kuwa na watumiaji milioni 20 wa intaneti na wengi wakiwa vijana hasa wanaoishi maeneo ya mijini. Kwa maana hiyo basi, vijana wengi hapa nchini wana fursa ya kutumia mitandao ya kijamii kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitawaletea faida katika maisha yao ya kila siku pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Kwa kuona hilo, serikali inatakiwa kufanya jitihada za kujenga miundombinu na kuweka mazingira stahiki ili watanzania wengi zaidi wapate fursa ya kutumia mitandao hii kujifunza na kushiriki katika mijadala itakayowaongeza ujuzi na maarifa, hivyo kuweza kuinua kiwango chao cha maisha. Serikali pia inatakiwa kuhakikisha mitandao ni mahali salama kwa biashara na kuepuka vitendo vya wizi na utapeli.