Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara zote zinazohusika na sekta ya viwanda, Ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya na mamlaka za serikali za mitaa pamoja na sekta binafsi kutambua na kufanyia kazi vikwazo dhidi ya ujenzi na ustawi wa viwanda nchini. Waziri Mkuu ameagiza hayo wakati akifunga wiki ya maonyesho ya viwanda yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani na kumuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuwasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa juu ya kampuni ya Budget Motors walioomba kibali cha kutengeneza na kuunganisha bodi za mabasi tangu mwaka jana.
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imeamua kujenga uchumi wa viwanda utakaokuwa mhimili mkuu wa maendeleo ya taifa na wananchi, hivyo itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ajenda ya ujenzi wa viwanda inafanikiwa”. Ameeleza Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema katika kupunguza vikwazo na kuboresha sera nchini, Rais Magufuli ameweka msukumo wa kutosha ili kurahisisha na kuboresha shughuli zote za kibiashara, lakini pia kuboresha sera za taifa za kodi kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani huku akiongeza kuwa, uwepo wa viwanda nchini utasaidia kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
“Huu ndio mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano unaolenga kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”. Amesema Majaliwa.