Home FEDHA Misaada imepungua, nchi inapitia kipindi kigumu-Dk. Mpango

Misaada imepungua, nchi inapitia kipindi kigumu-Dk. Mpango

0 comment 92 views

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema kufuatia wafadhili kupunguza misaada huku ile iliyosalia ikiwa na masharti, yakiwemo ya kukubali ushoga, nchi hivi sasa inapita kwenye kipindi kigumu. Dk. Mpango amesema hayo jijini Dodoma wakati akifunga mkutano kati ya Wizara hiyo na watoa huduma za serikali katika ukusanyaji mapato na kueleza kuwa, misaada imeporomoka sana na hata ile iliyobaki ina masharti mengi ya ovyo.

“Mtakuwa mmesikia jinsi ambavyo sasa wanafika mahali, hata bila aibu, wanasema sisi tuvumilie ushoga, Mnakubali? Mnakubali niende kuomba hela ya nchi halafu kuchekelea ushoga hata mbuzi hawafanyi? Tukipeleka jeshi letu kudhibiti magendo, wanasema tunarudisha nyuma biashara ya usafirishaji hapa nchini. Inawezekana? Kwa hiyo ninachotaka kuwaambia ni nini? Marehemu Baba wa Taifa alitufundisha kwamba tumepata uhuru wa bendera, lakini tuna kazi ya kutafuta uhuru wa kiuchumi”. Amesema Waziri Mpango na kuongoza kuwa:

“Sasa hapo ndipo shughuli pevu lazima tujitegemee na ili tujitegemee serikali kuu, serikali za mitaa lazima zijielekeze kukusanya mapato ya ndani ndiyo maana yake hakuna nyingine.”

Dk. Mpango ameeleza kuwa, serikali ikidhibiti madini wanasema wanafukuza wawekezaji na kwamba wamechukua miaka 57 sasa inatosha.

“Ninachotaka kuwaambia salamu zangu, kila mtanzania popote alipo hasa nyie mliomo humu ndani kila mtu aweke Tanzania moyoni mwake. Ni lazima kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa nguvu zote na hasa kwa kutumia mfumo huu wa GePG (wa njia ya kielektroniki), lazima twende kisasa”. Alisema.

Waziri huyo amesisitiza kuwa mfumo huo utasaidia kupata mapato yote stahiki kwa ajili ya kuendesha serikali kuu pamoja na serikali za mitaa.

“Hakuna mjomba, mjomba anayekutakia ya ovyo ovyo namna hiyo hapana ‘enough is enough’ (inatosha). Kama mnaipenda Tanzania kila mtu akazane na kusimamia huo mfumo to the best of ability (kwa uwezo wake). Mzingatie mafunzo mnayopata, mzingatie sheria zote, tunaelewana? Nawasihi sana,” alisema.

Waziri Mpango amebainisha kuwa taifa limechelewa, hivyo lazima maji yapatikane kwa ajili ya kinamama, elimu ya watoto na lazima kujenga misingi imara ya uchumi.

“Tutaweza kama tutaweza kukusanya ipasavyo na kudhibiti mianya ya uvujaji mapato. Bahati nzuri zamani tulikuwa tunatumia watu kutengeneza mifumo ya kielektroniki lakini siyo huu,” alisema.

Waziri Mpango amesema mfumo wa GePG umetengenezwa na watanzania kwa hiyo wale waliokuwa wanakula kula walipwe kwa kutengeneza mifumo mibaya na wakicheleweshewa malipo kwa siku moja, wanaharibu mifumo.

“Tunawataka wale wanaotengeneza mifumo wahakikishe wanatengeneza mifumo, tambueni hakuna atakayejenga nchi zaidi ya watanzania wenyewe”. Amesema.

Aliwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa ajili ya mama Tanzania na wasiwe sehemu ya uharibifu wa hiyo mifumo.

“Kila mmoja hapa wizarani huwa nawaambia unapopewa jukumu la kuwatumikia watanzania tambua kuna watu milioni 58 kwenye mabega yako na wengi wao ni masikini.

“Utumwa sasa mwisho lazima tutembee kifua mbele. mzingatie mafunzo haya kwenye kazi zenu ili tujidai sasa ni taifa huru linalojiendesha lenyewe,” alisema huku akisisitiza kuwa anatamani katika bajeti ijayo, Tanzania ijitegemee bila kukopa.

“Mungu atakaponipa nafasi nisimame nitamke kuanzia sasa serikali yetu itajitegemea tutatafuta mikopo labda ya kibinadamu kama matetemeko na mafuriko, hiyo ndiyo tutaenda kutafuta nje lakini vinginevyo tufanye wenyewe na tunaweza”. Amesisitiza Waziri Mpango.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter