Home BIASHARA Makubaliano mapya Airtel, Serikali yasainiwa

Makubaliano mapya Airtel, Serikali yasainiwa

0 comment 119 views

Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano baina ya serikali na kampuni ya Bharti Airtel kuhusu umiliki wa hisa za kampuni Airtel Tanzania. Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametia saini kwa niaba ya serikali ya Tanzania huku Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil Mittal akitia saini kwa niaba ya kampuni hiyo.

Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi amesema katika makubaliano hayo kampuni ya Bharti Airtel imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51 na hivyo kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka Serikalini.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, baadahi ya maeneo ya makubaliano ni pamoja na serikali kupokea gawio la kila mwaka ambapo itakuwa ikipata Sh. 10 Bilioni, kufutwa kwa madeni yote ya kampuni ya Airtel yaliyokuwa yamefikia Sh. 1 Trilioni, Bharti Airtel itatoa Sh. 1 Bilioni kila mwezi kwa muda wa miaka mitano kuanzia Aprili 2019 ikiwa kama ishara ya nia njema na Bharti Airtel pia itatoa Sh. 2.3 Bilioni kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Sunil Mittal amesema amefurahishwa na makubaliano hayo huku akieleza kuwa, awali aliona kuna ugumu wa kufikia makubaliano lakini baadaye alielewa kuwa lengo la Rais Magufuli ni kuhakikisha anaweka muelekeo mzuri wenye manufaa kwa taifa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter