Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanry amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kusafirisha tumbaku kuanzia saa kumi na mbili jioni kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Mwanry ametoa onyo hilo baada ya kukutana na wadau mbalimbali wa zao hilo mkoani humo na kuongezea kuwa watakaoruhusiwa kusafirisha tumbaku ni wale wanaoipeleka kuchakatwa mkoani Morogoro tu.
Mwanry amesema onyo hilo linatokana na vitendo vya baadhi ya wakulima na wajasiriamali wa zao hilo kukithiri hivyo hali hiyo imepelekea yeye kumuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Wilbrod Mtafungwa kuhakikisha kuwa hakuna tumbaku itakayotoka nje ya mkoa wa Tabora kuanzia saa kumi na mbili jioni na kuendelea.
Amewaambia wadau, wakulima na wafanyabiashara wa Tumbaku kuwa wanachotakiwa kufanya ni kuuza mazao yao katika vyama vya ushirika na Amcoss. Wakati huo huo pia, ameagiza vyama vya ushirika kuhakikisha viongozi wake wana elimu ya kutosha kwani kufanya hivyo kutapelekea viongozi hao kufanya kazi zao za ushirika kwa uelewa mkubwa zaidi.