Ni ukweli usiopingika kuwa hali ngumu ya maisha, kukosekana kwa kipato cha uhakika kumesababisha wananchi wengi kuishi kwa kutegemea mikopo kutoka sehemu mbalimbali rasmi na zisizo rasmi.
Ipo ile ambayo hutolewa na taasisi za fedha kama benki, vikundi vya kuwezeshana na mingine hutolewa na watu binafsi.
Mikopo hii kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikisababisha changamoto mbalimbali miongoni mwa jamii hususani pale mkopaji anaposhindwa kulipa mkopo.
Wananchi wengi hawana elimu ya fedha na hujikuta wakiingia katika matatizo na taasisi au watu binafsi wanaotoa mikopo.
Kukosekana kwa kipato cha uhakika, kumefanya watu wengi kutegemea mikopo hususani ile isiyo rasmi. Hali hii imewafanya baadhi ya watu kuwekeza fedha zao katika kutoa mikopo kwa riba ndani ya jamii.
Baadhi ya watu wamejikuta katika madeni na wengine wamepoteza mali zao kutokana na kushindwa kurejesha mikopo hiyo ambayo asilimia kubwa hutolewa na watu binafsi.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewatahadharisha Watanzania juu ya huduma za mikopo zinazotolewa na taasisi, makampuni au watu binafsi nchini.
Taarifa ya Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba inasema kwa mujibu wa Sheria ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2018 kifungu cha 16 (1) ni kinyume cha sheria kujihusisha na biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni.
“Katazo hili linajumuisha utoaji wa mikopo kwa njia mbalimbali ikiwemo utoaji wa mikopo kwa njia ya kidigitali bila kuwa na leseni,” ameeleza Tutuba.
Ameeleza kuwa umma unapaswa kutambua kuwa chini ya kifungu cha 17 cha sheria hiyo, Bo Tina mamlaka pekee ya kutoa leseni kwa taasisi, makampuni au watu binafsi wanaojihusisha na kutoa mikopo.
Taarifa hiyo imewataka wananchi kusoma kwa makini na kuelewa makubaliano wanayoingia na wakopeshaji ikiwa ni pamoja na kuelewa masharti ya mkopo na kuhakikisha kwamba mkopeshaji ana leseni halali ya kufanya biashara ya kukopesha.
Gavana Tutuba anaeleza kuwa mkopaji anapaswa kupewa nakala ya mkataba uliosainiwa kwa njia sahihi na nakala hiyo inapaswa kutolewa kila mkopeshaji anapotoa mkopo mpya.
“BoT inaendelea kuusisitiza umma kujiepusha kufanya biashara na taasisi, makampuni au watu binafsi wanaotoa huduma za kukopesha bila kuwa na leseni halali na kuwataka wananchi kutoa taarifa za makampuni, taasisi na watu binafsi wanaofanya biashara hiyo bila kuwa na leseni,” amesema Gavana Tutuba.