Home BENKI AfDB yaimwagia Tanzania mabilioni kutekeleza miradi ya maendeleo

AfDB yaimwagia Tanzania mabilioni kutekeleza miradi ya maendeleo

0 comment 90 views

Na Grace Semfuko-MAELEZO.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imesaini mikataba mitatu na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ya kuipatia msaada na mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya dola za Kimarekani 156.59 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 358.236 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mikataba hiyo ya mikopo na msaada imesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt Alex Mubiru ambapo kwa upande wa mikopo serikali ya Tanzania itailipa kwa kwa muda wa miaka 40 ijayo.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa 400kV kuanzia Nyakanazi Biharamuro mkoani Kagera hadi Kigoma uliopata mkopo  wa Dola za Kimarekani milioni 123.39, Mradi wa kudhibiti sumu kuvu kwenye mazao ya nafaka ambao umepata Dola milioni 33 zikiwepo Dola milioni 20 za msaada na Dola milioni 13 za mkopo huku bajeti ya serikali ya mwaka 2018/2019 nayo ikiongezewa mkopo wa masharti nafuu wa Dola milioni 56 sawa na Shilingi Bilioni 128.28.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo mitatu ya mikopo na msaada kati ya Tanzania na Benki ya maendeleo ya Afrika AfDB, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw.Dotto James amesema serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili kuwaletea maendeleo watanzania.

“Ndugu zangu hii ni hatua kubwa na nzuri kwetu watanzania, hizi sio fedha ndogo, ni fedha nyingi ambazo ni mkopo wa masharti nafuu pamoja na msaada kwenye eneo la kudhibiti sumu kuvu za nafaka, tutalipa mikopo hii kwa muda wa miaka 40” alisema Dotto James Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dkt Alex Mubiru amesema Benki hiyo inalenga kuimarisha maendeleo ya watanzania kwani fedha hizo zinaingia moja kwa moja kwenye miradi ambayo itatumiwa na wananchi.

“Benki yetu ya Maendeleo ya Afrika AfDB inalenga kuimarisha maendeleo ya wananchi, tuna miradi mingi tunayofadhili kwa nchi za Afrika, kwa Tanzania pia tunayo miradi tunayoimarisha, lengo la mikopo na misaada hii ni koboresha maisha ya watanzania” alisema Dkt Mubiru Mwakilishi Mkazi wa AfDB.

Zanzibar ni miongoni mwa eneo litakalonufaika na msaada huo kutoka Benki ya AfDB kwa upande wa kudhibiti sumukuvu kutoka kwenye mazao ya nafaka ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw.Ahmad Kassim Haji amesema watahakikisha wanalinda na kuhifadhi vizuri mazao yote ya nafaka na kwamba mradi huo utawawezesha kufanya shughuli hiyo kikamilifu.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter