Hivi karibuni Tanzania imepitia mabadiliko makubwa katika sekta ya uchumi na biashara kwa ujumla,mabadiliko haya yamesababishwa na kudorora kwa uchumi na hivyo kusababisha biashara nyingi kufungwa na zingine kusuasua.
Moja ya sekta zilizoathirika na hali hiyo ni sekta ya fedha,ikumbukwe hii ni sekta muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa nchi kwa ujumla. Fedha ndiyo sekta inayoangaliwa zaidi katika kuchambua vigezo vya ukuaji wa uchumi katika nchi nyingi duniani.Thamani ya fedha ikiwa juu basi na uchumi wa nchi hiyo utakua na kustawi.
Mabenki ni moja ya taasisi zilizo katika sekta hii ya fedha na ni waathirika wakubwa wa hali hii ya kiuchumi.Baadhi ya benki zimeanza kuchukua hatua ili kukabiliana na hali hii huku baadhi kama Covenant Bank for Women, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank zikifungwa na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu wa Benki kuu ya Tanzania(BoT).
Katika moja ya hatua zilizochukuliwa na taasisi hizi za fedha ni kushusha riba katika mikopo ili kutoa unafuu kwa wateja wao na pia kuvutia biashara. Hatua hizi zilianzia kwa Benki kuu ya Tanzania ambayo ilishusha riba ya fedha kwa taasisi za mikopo kutoka 16.0% mpaka 9.0% na pia ilipunguza kiwango cha amana zinazotakiwa kuwekwa na taasisi hizo BoT kutoka 10.0% mpaka 8.0%.
Hali hiyo ilifuatiwa na benki za CRDB na NMB ambazo nazo zilishusha riba ili kukabiliana na changamoto hiyo. CRDB walishusha riba kwa wafanyakazi kutoka 22% mpaka 16% na kuongeza kiwango cha mkopo kutoka milioni 50 mpaka milioni 100 huku muda wa marejesho ukipaa kutoka miaka 5 mpaka 7. NMB nayo iliamua kushusha riba kwa wafanyakazi kutoka asilimia 21 mpaka 19 na ikishusha riba ya wajasiriamali wadogo kutoka asilimia 23 mpaka 21 na huku ikiongeza muda wa marejesho kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa kutoka miezi 60 mpaka miezi 72.
Sina shaka ushushaji huu wa riba utakwenda kuvutia wakopaji hasa wajasiriamali wadogo na wafanyakazi ambao wengi wao pia ni wanachama wa vikundi vidogo vya mikopo maarufu kama Vicoba. Wakina mama wengi licha ya kuwa na ajira rasmi baadhi yao ni wanachama wa Vicoba.
Waajiriwa hawa wa taasisi za serikali na sekta binafsi zenye mshahara wa kati na mikubwa kulingana na umaarufu na msukumo wa jamii wengi wamejikuta ni wanachama wa Vicoba na ni wakopaji wakuu wakitumia ajira zao kama dhamana ya mikopo hiyo. Wengi hukopa na vikundi huwa na imani ya kuwakopesha kwa maana ya hata biashara zikiyumba basi mshahara utafidia rejesho.
Kushuka huku kwa riba bila shaka kunaenda kuwavutia wafanyakazi na wajasiriamali hawa ambao wengi ni wadau wa Vicoba na hivyo wataweka msisitizo zaidi katika kurejesha mikopo ya mabenki na Vicoba kudorora. Wadau hawa licha ya kukopa pia ni wawekaji wazuri wa amana(hisa) katika Vicoba vyao kitu ambacho huchagiwa na kipato wanachopata kupitia mishahara yao.hivyo ukopaji katika taasisi zingine za fedha bila shaka kutaathiri ushiriki wao katika vicoba kwa asilimia kubwa.
Wajasiriamali na wafanyakazi wawe makini katika kutumia fursa hii ya kushuka kwa riba ili kuepuka mrundikano wa mikopo hivyo kuwawia vigumu kuirejesha na hivyo kuathiri upande mmoja hasa ule ambao njia zake za kukopa zina masharti nafuu.