Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Abdul Zuberi amesema mamlaka hiyo itachukua hatua za kisheria kwa wafanyabiashara ambao watabainika kutotoa risiti za manunuzi kwa wateja wao. Zuberi amesema hayo mkoani Mbeya wakati wa kikao baina ya watumishi wa TRA na wafanyabiashara na kueleza kuwa, kitendo cha wafanyabiashara kutotoa risiti ni kuibia serikali mapato na sio uzalendo.
“Kama kuna mfanyabiashara yeyote ambaye anauza bidhaa zake bila kutoa risiti aache mara moja ukikamatwa utakuwa na kesi ya kujibu kuhusu uhujumu uchumi, nawashauri zingatie kanuni na Sheria zilizowekwa kwenye kodi ili mfanye biashara zenu kwa uhuru”. Amesisitiza Naibu huyo.
Pamoja na kuwataka wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa kuzingatia Sheria, Zuberi pia amewashauri kuwa makini wakati wanalipa kodi kwa watu wanaokusanya kodi moja kwa moja kwenye maeneo yao ya biashara na ikiwezekana, wawasilishe malipo hayo kwenye ofisi za TRA kwani baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwaibia.
“Mfanyabiashara kama una mashaka na mtumishi anayekusanya kodi usimpe badala yake fika kwenye ofisi za mamlaka ndipo utoe na uhakikishe unapewa risiti”. Amesema Zuberi.