Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amewahakikishia wafanyabiashara wa mafuta kutoka nchini Uganda kuwa, serikali imejipanga kutatua changamoto zote katika usafirishaji ili kushusha gharama za uchukuzi baina ya mataifa hayo mawili. Mhandisi Nditiye amesema hayo katika kikao maalum kilichowakutanisha wafanyabiashara wa mafuta wa Uganda na taasisi za uchukuzi kutoka Tanzania na kuongeza kuwa, serikali inatekeleza hayo kwa kuboresha miundombinu ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya biashara.
“Niwahakikishie kuwa changamoto zote zilizoainishwa baada ya majumuisho ya ziara yenu ya siku 5 nchini tutazifanyia kazi”. Amesema Naibu Waziri Nditiye.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ikiwemo upanuzi wa bandari, ukarabati wa reli na meli ili mizigo inayokwenda nchini Uganda kupitia bandari ya Dar es Salaam ifike kwa wakati muafaka.
Kwa upande wake, Mchumi Mwandamizi wa Wizara ya Ujenzi ya Uganda, Gerald Akini amemuahidi Naibu Waziri kuwa atafikisha katika ngazi husika yale ya kisera yanayohusu Uganda ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara. Mchumi huyo pia ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwapokea wafanyabiashara wa Uganda na kuweka mazingira mazuri ili watumie Bandari ya Dar es Salaam.