Rais wa Kenya William Ruto amewataka Wakenya kuwa na utamaduni wa kuweka akiba hususani kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Sisi ni miongoni mwa nchi za mwisho katika kuweka akiba katika bara letu, hamuwezi kuamini. Kwa sasa tuna takribani akiba ya 1.5 trilioni ambayo ni kiwango kidogo sana, mnajua hivyo?. Hatuna namna zaidi ya kubadilisha hii nchini na sisi ndio wa kuibadili,”
Rais Ruto ameeleza hayo siku chache baada ya kuapishwa kuwa Raisi wa tano wa nchi hiyo.
Ametolea mfano wa Tanzania na kusema ingawaje Kenya wameizidi kiuchumi, lakini Tanzania ina utamaduni mzuri wa kuweka akiba.
Ameeleza kuwa wataalamu wetu watakutana na watu wa NSSF ili kuangalia ni nini cha kufanya.
Amesema ingawa Tanzania ina uchumi mdogo ukilinganisha na Kenya lakini imewazidi kwenye utamaduni wa kuweka akiba.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ameandika “tuna kila sababu ya kujivunia utamaduni mzuri wa kuweka akiba.
Ni muhimu tudumishe utamaduni wa kuweka akiba katika taasisi za fedha iwe benki au mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa una faida kubwa katika uchumi na ustawi wa jamii.
Kwa sasa mfuko wetu wa PSSF una thamani ya shilingi Trilioni 8.6 na mfuko wetu wa NSSF una thamani ya shilingi Trilioni 6.2.
Hongereni wote mnaochangia katika mifuko hii na mnaoweka akiba katika taasisi za fedha.”