Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Zanzibar, Ali Suleiman Ameir amesema imejipanga kuwainua kiuchumi wajasiriamali ili kupambana na tatizo la ajira. Ameir amesema hayo wakati akifunga maonyesho ya kwanza ya kazi za wajasiriamali yaliyoandaliwa na Mtandao wa Tamaduni za Kijamii visiwani humo na kuongeza kuwa kuanzishwa kwa mfuko wa uwezeshaji, idara ya programu za uwezeshaji pamoja na vituo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ujasiriamali kumesaidia vijana kupata mbinu za kujiajiri.
“Hivi sasa vijana wengi wamejiajiri katika ujasiriamali baada ya kuona kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ajira”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha, ametoa wito kwa wajasiriamali kutokatishwa tamaa na matatizo yanayowakabili, na kuwataka kuongeza juhudi ili kufikia malengo yao. Vilevile, amewashauri wananchi kuthamini bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ndani badala ya zile zinazotoka nje.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Tamaduni za Kijamii Zanzibar, Ameir Abdallah Ameir amesema sekta ya ujasiriamali inakumbwa na chagamoto mbalimbali zikiwemo soko la uhakika, fedha na uhaba wa vifungashio.