Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Mb) amesema Benki ya Ushirika Tanzania (CBT) itakuwa chombo muhimu cha majadiliano na makubaliano ya kibiashara kati ya wakulima na Benki za Kibiashara.
Bashe amesema hayo Oktoba 17, 2024 katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wananchama wa Benki ya Ushirika Tanzania (CBT) uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri Bashe amesema CBT inaanza na mtaji wa Shilingi Bilioni 52 ambapo Makao Makuu yake ni jijini Dodoma na tayari ina matawi mkoani Kilimanjaro na wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.
Ameongeza kuwa benki hiyo inatarajia kuwa na matawi katika mikoa ya Tabora, Mtwara na Kagera kama sehemu ya malengo ya kutekelezwa na uongozi wa benki hiyo ambayo yanatakiwa kufikiwa ifikapo mwezi Juni 2025.
Waziri Bashe amesema benki hiyo itakuwa miongoni mwa benki kubwa nchini kwani miongoni mwa fursa za kukua kwa benki hiyo ni uwepo wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACOSS), Vyama vya Msingi (AMCOS) pamoja na Vyama Vikuu vya Ushirika (Cooperative Unions) ambavyo vipo kote nchini.
Amefafanua kuwa ofisi za vyama vya akiba na mikopo, ofisi za vyama vya msingi na ofisi za vyama vikuu vya ushirika zinaweza kutumika kama wakala wa Benki ya Ushirika.
“Benki hii itakuwa chombo chetu cha kutusadia sisi kama wakulima na vyama vya ushirika kujadiliana kibiashara na benki za kibiashara na hatimaye tutapata makubaliano ya kibiashara yenye faida,” ameeleza Waziri Bashe.