Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewaasa wakulima kujiunga katika vikundi ili kuwarahisishia ukusanyaji wa mahindi mengi na kuiuzia serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mkoani humo.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Memya wilayani Sumbawanga, Rukwa katika ziara ya siku mbili ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani humo, amesema haridhishwi na mfumo wa ununuaji wa mazao mkoani humo kupitia walanguzi, na hivyo kuwataka wananchi wajiunge na vikundi ili serikali iweze kununua mazao yao kwa urahisi.
Soma Pia Kero hizi zitatuliwe kuinua kilimo
Wangabo alisema kuwa ukifika wakati wa ununuzi wa mahindi, wanaoiuzia serikali ni watu binafsi hasa wafanya biashara ambao hulangua mahindi hayo kwa bei ndogo kwa wakulima na kuiuzia serikali kwa bei kubwa hivyo kuwanyonya wakulima ambao wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika shughuli za kilimo.
Akitoa maagizo kwa wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na walanguzi mkoani humo Wangabo amewataka walanguzi kuacha mara moja kununua mahindi kwa wakulima na badala yake akaagiza Wakala wa Hifadhi na Chakula kufanya kazi hiyo ili kutokomeza ukandamizaji unaofanywa na walanguzi hao.
Soma Pia Mafunzo yatolewa kuwanoa wadau wa kilimo
Nataka niagize NFRA kuwa ni marufuku katika mkoa wangu kununua mahindi ya walanguzi na kuwaacha wakulima wakikosa soko kwani hawa ni vigumu kutafuta soko wao wenyewe, lakini walanguzi wananweza kwenda kuuza hata katika masoko ya nje ya mkoa” Alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, John Msemakweli amesema kuwa serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ili kuboresha miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi na sekondari licha ya kupata mwitikio mdogo toka kwa wananchi.