Serikali imesema inaunga mkono jitihada za Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk Reginald Mengi za kuanzisha nchini maabara ya kisasa ya kutumia tiba ya seli shina (Stem Cell), kwa madhumuni ya kutibu magonjwa mbalimbali yasiyo na tiba hadi sasa.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr Faustine Ndungulile ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu tiba ya seli shina ( stem cells) kwa magonjwa ambayo hadi sasa hayana tiba.
Amesema licha ya kuwa Tanzania imeiboresha sana sekta ya afya kuna umuhimu jitihada hizo za serikali kuungwa mkono na wadau wa sekta binafsi.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi kufungua kongamano hilo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP limited Dr Reginald Mengi amesema kusudio lake la kuanzisha maabara hiyo ya utafiti wa kisasa ni kutoa mchango wake katika kuiwezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa ya binaadamu ambayo hayana tiba kwa sasa.
Aidha Mratibu Mipango wa Kampuni ya IPP Research, Technology and Innovation iliyoandaa kongamano hilo, Dr. Michael Magotti, na mwenzie Dr Kampon Sriwatanakul wamesema wanakusudia kuleta wazo jipya kuhusu tiba nchini na kwamba wameshapeleka maombi serikalini ya kuomba vibali vya kuanzisha maabara hiyo na lengo la kongamano hilo ni kuongeza uelewa kuhusu aina hiyo mpya ya matibabu kutoka kwa madaktari wabobezi kutoka nchi mbalimbali duniani.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na tiba, huku kukiwa na mamilioni ya watu wenye ulemavu mbalimbali barani Afrika wakibaki majumbani kwao kwa kukosa uwezo wa kupelekwa India au nchi nyingine zilizoendelea ili kupatiwa matibabu.