Kampuni ya Kiluwa Group, inategemea kujenga kiwanda cha mabehewa ili kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchangia harakati za serikali kutimiza lengo la kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohammed Kiluwa ameeleza hayo wakati wa hafla za kupeana nyaraka za makubaliano na kampuni ya Africa Jambo Group iliyopo Afrika Kusini. Katika maelezo yake, Kiluwa amesema kuwa kiwanda hicho kitajengwa mkoani Pwani katika eneo la uwekezaji la Kiluwa Free Processing Zone na kitatumia takribani Dola za Marekani milioni 150, ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 360 za kitanzania.
“Hiki tunachotaka kukifanya hakijawahi kufikiriwa na wengi, lakini kitaleta tija katika uchumi wa nchi. Tunafahamu tunapoelekea ni Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati. Tutahitaji mbinu bora za usafirishaji malighafi na bidhaa, reli ni njia rahisi na salama kusafirishia mizigo”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha Kiluwa ameelezea kuwa kiwanda hicho kimelenga kuwanufaisha watanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Afrika kwa ujumla. Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa utekelezaji wake utafanyika kwa awamu tatu huku kila awamu ikitoa ajira kwa watu takribani 980.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Jambo Group, Marthinus Christian Landman, amesema kuwa wapo tayari kuwekeza Tanzania kwa sababu ni sehemu salama na wamehamasishwa na sera ya viwanda ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.
“Siku zote mfanyabiashara anaangalia eneo ambalo atanufaika,tunaangalia zaidi faida kabla ya kukamilisha mikataba tumejiridhisha kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi na salama kiuwekezaji kwa sababu Rais John Magufuli amedhamiria kuona watu wanafanya kazi, hakuna kona kona wala rushwa”. Amesema Mwakilishi huyo.