Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Anthony Mavunde amemuagiza Kamishna wa kazi kukipeleka mahakamani kiwanda cha Uchapishaji cha Five Star kwa tuhuma za kuwaajiri raia wa kigeni wasio na vibali vya kazi.
Mavunde ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam na kuagiza kukamatwa kwa mwajiri wa kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wanne wa kigeni waliojificha baada ya kupata taarifa ya uwepo wa Waziri kiwandani hapo.
“Wameajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi ambao hawana vibali vya kazi, nafasi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania. Kamishna wa kazi hawa inabidi tuondoke nao ili sheria ifuate mkondo wake wote wapelekwe polisi hivi sasa” Alisema Mavunde.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri huyo amekitoza kiwanda hicho faini ya Sh.23.5 Milioni kutokana na mapungufu mbalimbali yaliyokuwepo ikiwa ni pamoja na wafanyakazi kutokuwa na mikataba.
Mbali na kiwanda hicho, Mavunde pia ametoza faini ya Milioni kwa kiwanda cha kutengeneza mabegi cha Matrix kilichopo Chang’ombe kwa madai ya kushindwa kufuata taratibu za afya na usalama.