Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema serikali haitatoa kazi za ujenzi wa barabara kwa kampuni ambazo hazijitoshelezi kifedha. Kamwelwe amesema hayo Bunda mkoani Mara baada ya kufanya ukaguzi katika ujenzi wa barabara ya Bulamba- Kisorya na kugundua kuwa, kampuni ya Nyanza Road Works iliyopewa tenda hiyo ina uwezo mdogo kifedha, hali inayopelekea kuchelewesha mradi huo.
Kamwelwe ametaja changamoto nyingine inayochelewesha mradi ni kampuni ya Inter Consult iliyofanya usanifu wa barabara kukosea michoro ya mradi huo, hivyo kupelekea mkandarasi kushindwa kufanya kazi inayotakiwa kikamilifu.
“Aliyesanifu mradi huu hakufanya vizuri na hivyo kumsababishia mkandarasi kuongezewa muda wa kazi miezi 35 mingine kutokana na kuongezeka kwa makalvati katika barabara hiyo na ukubwa wa tuta la barabara”. Ameeleza Waziri huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Mara, Mlima Ngaile, ametoa ahadi ya kumsimamia mkandarasi huyo kikamilifu na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango.