Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema serikali ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo (JICA) zimesaini mkataba wa mradi wa ujenzi wa daraja la Gerezani, ambao ukikamilika, utapunguza msongamano kwa kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya utiaji saini mkataba huo, Waziri Kamwelwe amesema mradi wa Gerezani ni muendelezo wa utekelezaji wa ilani ya serikali ya awamu ya tano kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu nchi nzima.
“Rais John Magufuli anatekeleza ahadi alizowaahidi wananchi, utiaji saini huu inaonyesha wazi serikali ina mahusiano mazuri na mataifa mengine hata wahisani wana imani na fedha wanazozitoa zinavyotumika”. Amesema Waziri huyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mhandisi Patrick Mfugale amesema mradi huo utakaogharimu Sh. 25.28 bilioni utatumia muda wa miezi 24 hadi kukamilika na kufafanua kuwa, ujenzi huo ni sehemu mkakati ya kupunguza msongamano. Daraja hilo la urefu wa mita 40, upana na sentimeta 30.4 na njia sita kwa ajili ya magari litajengwa na kampuni ya Sumito Mitsui Construction (SMCC).
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini, Toshio Nagase amesema utiaji saini mkataba huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Shirika hilo, Shinichi Kitaoka alipotembelea Tanzania mwaka 2017.