Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa ametoa wito kwa waandisi hapa nchini kuungana na kuwa kitu kimoja kwani kufanya hivyo kutaisukuma serikali kuwapa miradi mikubwa zaidi. Kwandikwa ametoa ushauri huo wakati akifunga mkutano wa mwaka wa wahandisi na kuwasisitiza wahandisi hao kufanya kazi na kuzingatia maadili yaliyopo ili kutekeleza miradi kwa viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Kwandikwa amesisitiza kuwa taaluma ya uhandisi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
“Shughuli ya uhandisi ni skeleton ya nchi, ni muhimu kwa uchumi wa nchi. Bodi inahitaji kusimamia maadili ya wahandisi, wapo wahandisi ambao wamesimamishwa kazi kwa kukiuka maadili ya kazi yao”. Amedai Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia kuhusu jitihada zinazofanywa kuwawezesha wazawa. Naibu Waziri Kwandikwa amesema mchakato wa kuwawekea utaratibu wa kisheria wahandisi kutoka nje umeanza. Katika utaratibu huo, imeelezwa kuwa wahandisi wa nje ya nchi watalazimika kufanya kazi kwa pamoja na wahandisi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya serikali.
Naye Kaimu Msajili wa ERB, Mhandisi Patrick Balozi amesema kutakuwa na mabadiliko katika kifungu cha 13 na 14 cha Sheria ya Bodi hiyo ili kutoa nafasi kwa wazawa kushirikiana na wahandisi wa nje kwenye miradi ya serikali.