Serikali ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya madini hususani katika kujengea uwezo watu wake, kubadilishana uzoefu, uongezaji thamani madini na kuwekeza kwenye kufanya tafiti mbalimbali ili kukuza sekta hiyo na kupanua mnyororo wa thamani ili kuongeza ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa.
Hayo, yameelezwa Januari 07 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young.
“Kwanza kabisa Balozi Young amefika ofisini kujitambulisha kwakuwa ana muda mfupi nchini tangu awasili lakini pia tumezungumzia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Tanzania na Uingereza.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania na Uingereza zimekubaliana katika kuwajengea uwezo watu wake na kubadilishana uzoefu hususani katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini (GST) na British Geological Survey (BGS) ya Uingereza ili kuwajengwa uwezo Watanzania kwakuwa na ujuzi stahiki katika masuala ya uendelezaji wa sekta ya madini,” ameeleza Waziri Mavunde.
Amebainisha kuwa, eneo la pili walilozungumza kwa urefu ni katika madini mkakati ambapo Uingereza wameonesha utayari katika kushirikiana na Tanzania katika eneo la mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini mkakati ambapo Tanzania imejipanga kuhakikisha inavutiwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini.
“Sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha madini ya kimkakati yanawanufaisha Watanzania na taifa, na ndiyo maana tumeandaa Mkakati maalumu wa kutekeleza azma hiyo huku ikizingatiwa kuwa madini hayo kwa sasa yana mahitaji makubwa duniani.
Tupo katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati huu maalum wa madini mkakati na muhimu ambao pia ni sehemu ya Kampeni ya Dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia matumizi ya nishati safi,” amesema Waziri Mavunde.