Maonesho ya saba ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yenye lengo la Kutangaza na kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa za Tanzania yamefunguliwa.
Maonesho hayo yaliyoanza Desemba 3 hadi 9 yanayofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es salaam yakiwa na kauli mbiu ya ‘nunuachakwetu’.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Omar Said Shaaban amezindua maonesho hayo na kusema ni nyenzo inayolenga kuwezesha na kuhakikisha Sekta ya Uwekezaji katika Viwanda na Biashara nchini inapata ustawi zaidi kwa kutambulisha bidhaa mpya sokoni ili zifahamike kwa walaji.
Amesema hiyo itawawezesha wazalishaji kupata mrejesho mzuri kutoka kwa wateja wao.
‘’ Maonesho haya yanalenga kuwaunganisha wanunuzi na wazalishaji kujenga uzalendo wa kununua bidhaa za Tanzania , kujifunza na kubadilishana uzoefu na teknolojia pamoja na kuongeza ajira zaidi hasa kwa vijana na wanawake’’ amesema Waziri.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis aameeleza kuwa maonesho haya yamelenga kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.
Nyingine ni kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma nyingine zinazohitajika viwandani, wasambazi wa teknolojia ya viwanda kutoka ndani na nje ya nchi, Taasisi za Uwezeshaji Biashara ili kujadili namna ya kutatua changamoto zinazoleta vikwazo vya uzalishaji na biashara, na kuongeza uelewa wa bidhaa za viwandaa zinazozalishwa nchini ili kupata masoko endelevu.
Ameeleza kuwa maonesho hayo yameendelea kupata muitikio mkubwa akibainisha kuwa idadi ya washiriki imendelea kuongezeka kutoka Washiriki 121 kwa mwaka jana hadi kufikia washiriki 502 kwa mwaka huu.