Katika kuwasaidia wakulima kwenye matumizi ya fedha hasa wakati wa mavuno, Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi za kifedha ikiwemo Benki Kuu, Taasisi za Uwekezaji na Bima zimeshauriwa kuanzisha kliniki ya elimu ya fedha kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, George Mbesigwe alipokutana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha.
Timu hiyo ipo mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi na makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na wanafunzi.
“Kipindi cha mavuno huku kwetu ndo kipindi ambacho wananchi wanakua na fedha, hivyo elimu hii ikitolewa wakati wa mavuno itasaidia wakulima kuhamasika kufungua akaunti benki, kufanya uwekezaji kupitia Taasisi za Uwekezaji au kukata Bima ya mazao kwakuwa zitakua zimefika katika eneo husika la mavuno,” amesema Mbesigwe.
Ameongeza kuwa uhitaji wa elimu ya fedha kwa wananchi ni mkubwa hivyo ni vyema zoezi hilo likawa endelevu ili kuhakikisha linawafikia wananchi wengi ili waweze kupanga matumizi sahihi ya fedha zao.
Naye Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Ruangwa, Edward Mbaruku ameahidi kuendelea kuwahamasisha wananchi wa Halmashauri hiyo kujenga mazoea ya kujiwekea akiba, kukopa katika Taasisi rasmi kuepuka migogoro lakini pia kusajili vikundi ili waweze kutambulika na Serikali na kuwa na sifa yakupata mikopo na fursa nyingine zinazotolewa na Serikali kupitia vikundi.
Salim Khalfan Kimaro ambae ni Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha amewashukuru wananchi wa Ruangwa kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa semina kwa kuuliza maswali na kutoa ushauri ambao utazingatiwa awamu nyingine ya zoezi la utoaji elimu ya fedha.
“Sisi kama Wizara ya Fedha tunaahidi kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu hii muhimu kwa kuwa itamsaidia kupanga bajeti, kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji na kujikwamua kiuchumi”, amesema Kimaro.