Home FEDHAMIKOPO BoT yaendesha mafunzo mfumo taarifa za mikopo Tanzania

BoT yaendesha mafunzo mfumo taarifa za mikopo Tanzania

0 comment 34 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendesha mafunzo kwa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu mfumo wa taarifa za mikopo Tanzania.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha washiriki kuhusu umuhimu wa mfumo huo na kuwahamasisha kuutumia kwa kutoa taarifa za wakopaji wao na kutumia taarifa hizo wanapochakata maombi ya mikopo ya wateja wao.

Mfumo wa taarifa za mikopo ni utaratibu wa kubadilishana taarifa za wakopaji miongoni mwa taasisi zinazotoa huduma za mikopo ili kuleta ufanisi katika sekta ya mikopo.

Semina hiyo, inayofanyika katika Tawi la BoT Mtwara kuanzia tarehe Desemba 02 hadi 06 2024, inahusisha pia ushiriki wa wawezeshaji kutoka kampuni za ukusanyaji wa taarifa za mikopo nchini, zikiwemo Credit Info na Dun & Bradstreet Tanzania.

Wawezeshaji hao watapata fursa ya kueleza shughuli zao kwa washiriki wa semina, ambao ni wawakilishi kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha katika mikoa ya Kanda ya Kusini.

Akitoa mada ya utangulizi, mtaalam kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Gwamaka Charles ameeleza faida za mfumo huo kuwa ni kuwepo kwa soko la mikopo lenye tija na ufanisi na kuchangia katika kukua kwa sekta ya fedha na uchumi nchini.

“Mfumo huu unapunguza ukosefu wa taarifa kati ya wakopeshaji na wakopaji ili kuwawezesha wakopeshaji kupata historia za waombaji wa mikopo kirahisi na kujenga nidhamu nzuri na uwajibikaji katika soko la mikopo kwa wakopeshaji na wakopaji,” ameeleza Gwamaka.

Ameongeza kuwa mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, hivyo kuchochea ajira, vipato, na ustahimilivu wa sekta ya fedha.

“Kuwepo kampuni zinazokusanya taarifa za mikopo, kunapunguza gharama na muda unaotumiwa na wakopeshaji kukusanya taarifa za wateja, na kusaidia kudhibiti athari za mikopo katika taasisi za kifedha ili kupunguza hatari ya kufilisika,”amesema.

Aidha, mfumo wa taarifa za mikopo unasaidia kutumia historia nzuri za mikopo kama mbadala wa dhamana ya mkopo na kupunguza gharama za kukopa (riba na gharama nyingine).

Washiriki wa semina hiyo wanatoka wilaya zote zilizoko katika mikoa ya Mtwara na Lindi na wengine kutoka sehemu nyingine.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter