Home BIASHARAUWEKEZAJI Mengi azindua kampuni ya kutengeneza simu

Mengi azindua kampuni ya kutengeneza simu

0 comment 164 views

Mwenyekiti wa IPP, mfanyabiashara na mjasiriamali maarufu nchini Tanzania, Dk. Reginald Mengi kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia ya Touchmate kutoka nchini Dubai, wametambulisha rasmi ujio wa kampuni mpya ya IPP Touchmate, kampuni ambayo itakuwa ya kwanza Tanzania, na itajikita katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki, ikiwemo simu za mikononi na kompyuta huku uwekezaji wake ukiwa zaidi ya Sh. 11 bilioni. Akizungumza na waandishi wa habari, Dk Mengi ameeleza kuwa simu hizo zitakuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa zaidi ya wiki moja, zikiwa ni maalumu kwa ajili ya mazingira yaliyo na changamoto ya umeme hasa vijijini.

Mbali na hayo, Dk. Mengi ameeleza kuwa wanatarajia kuzalisha ajira rasmi na zisizo rasmi takribani 2000, na kampuni hiyo itatoa kipaumbele kuajiri watu wenye ulemavu walio na sifa stahiki.

“Tunatarajia kutoa ajira zaidi ya elfu mbili rasmi na zisizo rasmi. Kwa namba hiyo tutaipunguzia serikali ya awamu ya tano mzigo wa kutoa ajira”. Amesema mfanyabiashara huyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Touchmate, Vasant Menghani amesema wanalenga kuzalisha ajira zaidi ya 200,000 katika kipindi cha mwaka mmoja na uzalishaji wao utakuwa kwa awamu.

“Awamu ya kwanza itakuwa ya simu, awamu ya pili tutazalisha tablets na awamu ya tatu tutazalisha vitabu vya mtandaoni na awamu ya mwisho itakuwa uzalishaji wa vifaa vya nyumbani”. Amesema Menghani.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter