Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema Halmashauri ya wilaya hiyo imetoa Sh. 42,630,000 kwa vikundi kumi na moja ikiwa ni makusanyo ya mapato ya ndani kama ambavyo serikali imeagiza kwa halmashauri zote nchini. Mwaisumbe aliyekabidhi fedha hizo amesema lengo ni kuwawezesha kiuchumi wananchi walio na hali ngumu kiuchumi na kuwashauri watakaonufaika na mkopo huo kurejesha ndani ya muda uliopangwa.
“Serikali imetoa mkopo huu bila riba, hivyo ni wajibu wenu kutumia na kurejesha ili iweze kuendeleza vikundi vingine vya wilaya”. Ameeleza Mwaisumbe.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema atashirikiana kwa karibu na watendaji wa halmashauri hiyo ili kuhakikisha kuwa vyanzo vipya vya mapato vinapatikana na kuendelea kuwatumikia wananchi kwa kuwapa mahitaji yao ikiwemo kuwawezesha kiuchumi.
“Niseme tu sina wasiwasi na halmashauri hii chini ya Mkurugenzi wake, Juma Mhina katika ukusanyaji wa mapato, niseme ninawapongeza na endeleeni kupiga kazi kwa kutetea maslahi ya wilaya na taifa”. Ameongeza Mkuu huyo wa wilaya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Longido, Juma Mhina amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kwa mara ya kwanza kutoa mkopo kwa asilimia 100 na kueleza kuwa wamepiga hatua kwani mwaka jana walitoa mkopo kwa asilimia 75 pekee.
“Miaka ya nyuma makusanyo yalikuwa madogo, ilikuwa Sh. 400 milioni ila kwa sasa tumepiga hatua kutoka hapo hadi Sh. 1 bilioni na kupitia mapato haya tunatoa asilimia 10 kutekeleza agizo la serikali”. Ameeleza Mhina.