Kufuatia uzembe uliopelekea kudorora kwa viwanda vya korosho hapa nchini. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph George Kakunda ametengua ukurugenzi wakurugenzi wawili waliokuwa wakisimamia viwanda na maghala katika wizara hiyo. Waziri Kakunda ameeleza kuwa baada ya kutembelea viwanda hivyo vilivyopo mkoani Lindi hadi Mtwara, amekutana na hali mbaya huku viwanda vingi vikiwa vimegeuzwa kuwa maghala.
“Nimeamua kumpunguzia majukumu ndugu Isaac Legonda, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda, ataripoti kwa Katibu Mkuu atapangiwa kazi nyingine ya uofisa. Nimemtafuta tangu juzi ili aweze kunipa habari za viwanda hayupo ofisini, Katibu Mkuu hana taarifa za kutosha huyu mtu yuko wapi. Katibu Mkuu atajua mwenyewe hatua zinazotumika katika kanuni za adhabu za utumishi”. Amesema Waziri Kakunda.
Mkurugenzi mwingine aliyevuliwa wadhifa wake ni Augustino Mbulumi aliyekuwa Mkurugenzi wa usimamizi wa maghala. Waziri huyo mpya wa viwanda amesema ametengua uteuzi wa Mbulumi kufuatia utendaji kazi hafifu na uzembe.
“Atateuliwa Mkurugenzi mwingine ambaye atakuwa tayari kuwajibika vizuri zaidi. Hatuwezi kuwa na watu ambao hawaendi na kasi ya Mheshimiwa Rais”. Ameeleza Waziri Kakunda.