Benki kuu ya Tanzania (BoT) imeiweka benki ya Bank M Tanzania Plc chini ya usimamizi wake kutokana na benki hiyo kuwa na upungufu wa fedha, kinyume na taratibu za sheria ya mabenki na taasisi za fedha. Akizungumzia suala hilo, Gavana na BoT Prof. Florens Luoga amesema benki hiyo imewekwa chini ya uangalizi kuanzia jana kutokana na uhaba wa fedha, hali ambayo amedai inahatarisha usalama wa sekta ya fedha na endapo ingeendelea, usalama wa amana za wateja wake ungeathirika.
“Umma unaarifiwa kuwa katika kipindi kisichozidi siku 90 kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma wa kibenki za Bank M zitasimama ili kuipa nafasi BoT kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili”. Ameeleza Prof. Luoga
Hata hivyo, Gavana huyo wa benki kuu amewataka wateja wa Bank M kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kutafuta ufumbuzi kwa kuwa maslahi ya walio na amana yatalindwa ili kuendelea kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.