Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa benki hapa nchini kupunguza viwango vya riba zinazotozwa kwenye mikopo mbalimbali inayotolewa kwa wananchi. Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Bomang’ombe wilayani Hai katika mkutano wa hadhara.
Waziri Mkuu mbali na kudai mazingira ya benki kutoza riba kubwa yanawapa wakati mgumu wajasiriamali kufikia malengo yao, pia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi hususani vijana, wanawake na walio na ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri na kusema kila halmashauri hapa nchini inapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na wananchi wenye ulemavu kupata mitaji.
Pamoja na hayo, Majaliwa ambaye anafanya ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro amewataka wakulima wa kahawa kubadilika na kutoa miti ya zamani na kupanda mipya ili kuongeza tija katika kilimo chao.