Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imetangaza kuwa kampuni ya Vodacom Group ya Afrika Kusini inatarajia kununua hisa zote zinazomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa hapa nchini, Rostam Aziz. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, tume hiyo imepokea maombi ya kununua asilimia 26.25 ya hisa za kampuni iliyokuwa inasimamia hisa hizo ndani ya Vodacom Tanzania ya Mirambo, ambayo inamilikiwa na Aziz.
Agosti mwaka jana, Vodacom Tanzania iliorodhesha asilimia 25 ya hisa zake kwenye Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) ili kutoa nafasi kwa watanzania kumiliki kampuni hiyo. Kutokana na mabadiliko hayo, Vodacom Group inaendelea kuwa mmiliki mkubwa wa Vodacom Tanzania (48.75) ikifuatiwa na Rostam (26.25) huku asilimia zilizosalia zikienda kwa wawekezaji wengine wadogo.
Vodacom Group ni kampuni tanzu ya Vodaphone kutoka Uingereza ambayo inatoa huduma za mawasiliano barani Afrika. Kampuni hiyo imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Johannesburg (JSE) na hivi sasa inamiliki asilimia 48.75 ya hisa zote za Vodacom Tanzania.