Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza yaani Julai hadi Novemba 2018, serikali imekusanya makusanyo ya ndani ya Sh. 7.37 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 88.9 ya makadirio ya Sh. 8.30 trilioni katika kipindi hicho. Waziri Mpango amesema hayo jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Katika maelezo yake, Waziri huyo amesema katika kipindi hicho, mapato ya kodi yalifikia Sh. 6.23 trilioni ikiwa ni sawa na asilimia 88 ya lengo la kukusanya Sh. 7.04 trilioni kwa kipindi hicho. Vilevile, mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh. 936.03 bilioni sawa na asilimia 21 zaidi ya lengo la Sh. 775.36 bilioni huku mapato ya halmashauri yakifikia Sh. 203.8 bilioni, sawa na asilimia 61 ya lengo.
Mbali na hayo, Dk. Mpango ameeleza kuwa ongezeko la mapato yasiyo ya kodi limetokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji kwenye taasisi, mashirika na kampuni kulikopelekea serikali kupata michango na gawio stahiki kutoka kwenye uwekezaji wake. Aidha, kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye wizara na idara zinazojitegemea kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG) ambapo kati ya Julai 2017 hadi Novemba 2018, takribani taasisi za serikali 325 zimetumia mfumo huo kukusanya maduhuli.
Kuhusu jitihada za kuboresha mazingira ya kufanya biashara, Dk. Mpango amesema serikali kupitia Sheria ya Fedha 2018/19 ilipunguza baadhi ya ada na tozo ambazo zilikuwa kero kwa wananchi zikiwemo za mazingira, TBS, TFDA na tozo kwenye madini ya chumvi. Kuhusu changamoto ya ukusanyaji mapato, Waziri huyo amesema hali hiyo inatokana na ukwepaji wa kodi, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa kudai risiti pale wanapofanya manunuzi na wafanyabiashara kutoa risiti pale wanapofanya mauzo pamoja na wigo mdogo wa kodi.