Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo amesema manispaa hiyo itaanza kutoa mikopo kwa wanawake, vijana pamoja na watu walio na ulemavu kwa kushirikiana na benki ya CRDB ambayo ilishinda tenda hiyo baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa ikiwemo riba ya asilimia nane ya mkopo.
Kutolewa kwa mikopo hiyo yenye thamani ya Sh. 1.9 bilioni ni harakati mojawapo ya utekelezaji wa agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa lengo la kuwezesha wananchi. Mbali na hayo, Kayombo ameeleza kuwa mikopo hiyo inatarajiwa kutolewa kwa kata 14 zilizopo katika manispaa hiyo kupitia vikundi vya ujasiriamali na amewataka wataobahatika kupata mikopo hiyo kutimiza malengo waliojiwekea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za benki mbadala wa CRDB Philip Alfred amesema mikopo hiyo itazingatia vigezo vilivyowekwa na manispaa ili kusaidia makundi hayo kupambana na umaskini na kupiga hatua za kujiletea maendeleo.