Mkoa wa Dodoma umetajwa kuwa na fursa nyingi za kilimo zinazoweza kuinua zaidi uchumi wa nchi kutokana na ardhi yake kukubali mazao mengi ya aina tofauti.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ameutaja mkoa huo baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi mkoani humo Agosti 22, 2024 baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Mashamba ya Pamoja na Skimu ya Umwagiliaji ya Bulid Better Tomorrow (BBT) Ndogowe.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameeleza kuwa hapo awali jamii iliaminishwa kuwa mkoa wa Dodoma ni jangwa ambalo linaweza kuzalisha mazao machache jambo ambalo siyo sahihi.
Amefafanua kuwa Dodoma inaweza kuzalisha mazao mengi yakiwemo mitende, mizaituni, mipera, parachichi na mikomamanga hivyo wakulima wachangamkie fursa ya kufanya kilimo cha mazao hayo ili waweze kujiongezea kipato.
Kuhusu mkoa kupata kiwango kidogo cha mvua, Dkt. Mpango amesema mkoa wa Dodoma una maji mengi chini ya ardhi yanayokidhi kilimo cha umwagiliaji.
Hivyo, amesema kuwa Serikali imewekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima wa mkoa wa Dodoma kuzalisha katika vipindi vyote vya mwaka pasipo kutegemea mvua.
Akizungumza katika mkutano huo wa Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ndiyo njia pekee ya kuboresha maisha ya idadi kubwa ya Watanzania.
Naibu Waziri Silinde amesema Wizara ya Kilimo pamoja na Wananchi wanaojishughulisha na kilimo wanamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa juhudi zake za kuwekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji kwani wakulima wataweza kuzalisha katika vipindi vyote vya mwaka pasipo kutegemea mvua.
Amefafanua kuwa katika wilaya ya Chamwino pekee Serikali inatekeleza miradi 8 ya umwagiliaji ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo imeongeza hamasa kwa wananchi wengi kujishughulisha na shughuli za kilimo.