Home VIWANDA Viwanda vidogo vinajiandaa vipi kuelekea Tanzania mpya ya viwanda?

Viwanda vidogo vinajiandaa vipi kuelekea Tanzania mpya ya viwanda?

0 comment 94 views

Tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani sekta ya viwanda imeboreshwa na kufanyiwa mabadiliko kwa kiasi kikubwa. Serikali imeweka azma ya kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuimarisha uchumi wake na kuzalisha ajira zaidi kwa vijana. Dhamira hii imeonekana kukubaliwa na kuungwa mkono na sekta mbalimbali hapa nchini. Lakini kabla ya kufikiria matunda yote yatakayotokana na uchumi wa viwanda inapaswa kujiuliza, viwanda vidogo pamoja na vile vya kati vimejipangaje kuelekea Tanzania hii mpya?

Ni dhahiri kuwa ili kukuza uchumi wa nchi kwa kupitia sekta ya viwanda ni lazima kutambua changamoto zilizopo katika sekta hii na kutafuta suluhisho la kudumu. Pia inatakiwa kufahamu kuwa asilimia kubwa ya viwanda hapa nchini ni vidogo na vya kati hivyo lazima kuwepo na mazingira mazuri yatakayopelekea viwanda hivi kuweza kuendelea na kuongez kasi ya uchumi wa viwanda.

Inatakiwa kujiuliza, viwanda vidogo na vile vya kati vimejipanga vipi kukabiliana na kasi ya serikali ya awamu ya tano katika kuinua uchumi nchini? Viwanda hivi vidogo vinapata misaada yoyote kutoka kwa serikali au wadau mbalimbali ili kuongeza mitaji yao, kuongeza maarifa yao pamoja na kuongeza uzalishaji wao? Serikali imefanya jitihada zozote ili kutatua changamoto zinavyopelekea viwanda hivi kuendelea kuwa katika hali ya chini?

Pia kuwe na mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji wa nje na hata hapa ndani. Kuweka mazingira mazuri ya kuwekeza katika viwanda vidogo ni njia moja wapo ya kuinua viwanda hivi na kuvisaidia kuendelea na kupiga hatua kimaendeleo. Wawekezaji wengi wamekuwa wakikimbilia kuweka fedha zao kwenye miradi mikubwa huku wakiviacha nyuma viwanda vidogo kutokana na kuwa katika mazingira ambayo sio mazuri kama ilivyo kwa viwanda vikubwa.

Ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo kupitia sera ya viwanda kama ambavyo serikali imedhamiria, ni vizuri kama viwanda vidogo vikitumia rasilimali walizonazo kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha zinazingatia viwango na ubora ili vipate fursa ya kustahimili ushindani katika soko la kitaifa. Bila ya kuwa katika ubora wa hali ya juu bidhaa hizo hazitofanya vizuri sokoni na hali hiyo inaweza kupelekea baadhi ya viwanda vidogo kushindwa kujiendeleza.

Sera hii ya kubadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda imepokelewa kwa mikono miwili katika jamii zetu. Lakini ni vizuri kama serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali pamoja na wadau wa masuala ya maendeleo ikiendelea kuelekeza nguvu nyingi zaidi kuinua viwanda vidogo ili vipate kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujiendesha na kukabiliana na Tanzania hiyo mpya. Kuviacha nyuma viwanda vidogo haitasaidia kasi ya uchumi ya viwanda hapa nchini kwani watanzania wengi nao watakuwa wameachwa nyuma.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter