Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI ‘Worknasi’ ichangamkiwe

‘Worknasi’ ichangamkiwe

0 comment 87 views

Changamoto ya ajira ipo kila mahali. Ni asilimia ndogo sana ya watu hubahatika kupata ajira moja kwa moja baada ya kumaliza masomo. Kutokana na hilo, watu mbalimbali wamekuwa wakija na mbinu za kuweza kutatua tatizo la ajira nchini. Kati ya harakati hizo ni pamoja na ugunduzi wa programu za kisasa ambazo ni rahisi kwa watu kuzifikia kutokana na matumizi ya kasi ya vifaa vya kielektoniki.

Edgar Mwampige, mwanzilishi wa programu inayoitwa “Worknasi” ni moja ya watanzania ambao wamelenga kutatua tatizo la ajira hapa nchini. Mwampige aliamua kuanzisha programu hiyo baada ya kugundua kuwa yeye mwenyewe anakosa fursa nyingi za kazi kutokana na kutokuwa na eneo maalum la kufanyia kazi zake, hivyo akaamua kuanzisha Worknasi ili kuweza kuwasaidia watu wengine ambao wanapitia changamoto hiyo.

Kupitia programu hiyo mtu yoyote barani Afrika, kwa kutumia simu au kompyuta anaweza kutafuta kazi, kuajiri wataalamu kulingana na mahali ulipo na muda utakaohitaji huduma yao, kupata nafasi/sehemu ya ofisi kulingana na mahali/muda unaohitaji kutokana na ratiba zako pamoja na kupata nafasi/sehemu kwa ajili ya kufanya vikao vya kazi.

Kwa lugha nyingine programu hii imerahisisha maisha na kuhakikisha kila mtu anafanya kazi zake na hata kwa wale wanaohitaji kazi za ziada, unaweza kujipatia fursa ya kufanya kazi kwa muda mfupi huku ukiendelea na shughuli zako nyingine, kwa kufanya hivyo inakurahisishia kukuza mtandao, unapata kipato zaidi, unajenga mahusiano na watu wa aina mbalimbali n.k.

Pia kwa wale wasio kuwa na uwezo wa kulipia maeneo ya ofisi kwa muda mrefu, hapa wanapata fursa ya kulipia maeneo ya ofisi kwa muda mfupi pale tu inapohitajika kufanya hivyo. Kwa mfano kama kuna mkutano, kama kuna wateja wa muhimu ambao ni lazima ukutane nao katika mazingira ya kiofisi basi unaweza kukodi nafasi ya ofisi na kukamilisha shughuli zako katika mazingira mazuri.

Pia programu hii ni fursa kwa wafanyabiashara wa majengo/wapangishaji. Kutokana na maeneo, wapangishaji wanaweza kujikita na upangishaji kwa ajili ya masuala ya kazi kama mikutano, nafasi ya ofisi nk ili kuweza kujipatia fedha.

Jambo la msingi linaloweza kufanyika ni kutoa elimu hasa kwa vijana kuhusu programu kama hizi ili kuweza kupunguza idadi ya watu wasio kuwa na ajira, kwani kuna watu wengi sana mtaani ambao wana ujuzi wa kutosha lakini hawana kazi. Kupitia programu kama Worknasi, vijana wanaweza kupata kazi na kutengeneza kipato ambacho kinaweza kuwasaidia katika uanzilishi wa miradi mbalimbali ya ujasiriamali.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter