Wakala wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) imeanza kusafirisha tani 36,000 za mahindi yaliyonunuliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwenda nchi za Sudani ya kusini na Uganda, ikiwa ni sehemu ya tani 160,000 ya chakula iliyonunuliwa na WFP mwaka 2018 kwa thamani ya Shilingi bilioni 132.2.
Aidha, NFRA imewataka wakulima kutumia fursa hiyo kuwauzia WFP mahindi, na pia kuhakikisha mahindi yao yana ubora ili kuepuka usumbufu wakati wa kuuza. Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Usafirishaji Chakula wa WFP, Mahamud Mabuyu amesema Tanzania ni moja ya nchi ambayo haitumii teknolojia ya Uhandisi Jinsi (GMO) ndio maana WFP wananunua mazao nchini hapa.
Pamoja na hayo, Shirika hilo limeweza kuwainua wanawake kwa kununua mazao kwao ambapo utafiti unaonyesha kuwa WFP imeweza kuwaunganisha wakulima wadogo 53,000 na NFRA na asilimia 44 kati ya hao ni wanawake.
Hivi karibuni Shirika la Reli Tanzania (TRC) ilipata msaada wa Shilingi bilioni 1.8 kutoka WFP kwa ajili ya kukarabati baadhi ya mabehewa hivyo. Meneja wa kituo cha TRC mjini Dodoma, Rose Gauga amesema wana uwezo wa kusafirisha mzigo huo hadi Uganda kwani kila behewa lina uwezo wa kubeba tani 40.