Mchakato wa kuchagua jina kwa ajili ya kampuni au biashara ni hatua muhimu kwani ni mwanzo wa mafanikio yako kama mfanyabiashara. Jina la biashara lina nafasi kubwa katika kuvutia soko na hivyo inapaswa kuwa makini. Wafanyabiashara wengi hawaweki mkazo kwenye suala hili kwa sababu hawafahamu uzito wake.
Yafuatayo ni makosa makubwa matatu kila mfanyabiashara anapaswa kuepuka wakati anachagua jina kwa ajili ya biashara yake:
- Usichukue maoni ya kila mtu. Kila mtu huwa na mawazo yake hivyo mfanyabiashara akiruhusu maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, kufanya uamuzi sahihi itakuwa changamoto. Badala ya kusikiliza maoni ya kila mtu, unaweza kuunda kikundi kidogo cha watu wa aina mbalimbali ambao watakusaidia kufanya uamuzi sahihi na kukupatia ushauri. Kufanya hivi kunarahisisha zoezi zima la kuchambua jina sahihi kwani maoni ni machache na hivyo yote yanaweza kuchambuliwa na kujadiliwa kwa umakini zaidi. Unapofanya hivi, hakikishi kundi hilo linajumuisha watu wa aina tofauti ili uweze kupata maoni ambayo hayafanani.
- Kosa la pili ambalo wafanyabiashara wengi hufanya ni kuunganisha maneno mawili kuwa moja. Katika wa zoezi la uchaguzi wa jina la biashara, unachotakiwa kufahamu ni kwamba kwa sababu una uwezo wa kuunganisha maneno pamoja haimaanishi kuwa unapaswa kufanya hivyo. Mara nyingi, maneno yaliyounganishwa yanachanganya hivyo ni rahisi kusahaulika. Inatakiwa kuwa mbunifu na kuhakikisha kuwa jina la biashara yako linaeleweka na haliwachanganyi wateja kwa namna yoyote ile.
- Hakikisha jina la biashara yako ni la kipekee na lina mvuto kwa wateja. Epuka majina ambayo yanaelezea kwa undani biashara yako inahusu nini moja kwa moja kwa kuwa mengi huwa marefu na hivyo kukosa ubunifu, jambo ambalo linaweza kusababisha wateja wasivutiwe na hivyo kununua mahitaji yao sehemu nyingine. Jina lako linatakiwa kuhamasisha wateja na sio kuwafukuza.
Kama unafikiria kuwa mfanyabiashara, ni muhimu kuzingatia haya ili kuhakikisha jina la biashara yako ni kivutio namba moja kwa wateja wako.