Mastercard ni kadi ya kielektroniki inayotumika kukamilisha miamala ya fedha. Kadi hiyo inaweza kuwa kadi ya mkopo, kadi yenye fedha za akiba au Prepaid.
Mtumiaji wa kadi hizi anaweza kulipia ua kufanya miamala ya fedha katika nchi nyingi duniani ikiwa ni pamoja na kulipia bidhaa au huduma katika duka au sehemu yoyote yenye mashine inayoruhusu huduma ya ulipaji kwa kadi.
Zifuatazo ni faida za kutumia Mastercard:
- Umiliki wa kadi hii humrahisishia mmiliki kufanya malipo kwa urahisi, na usalama zaidi katika sehemu mbalimbali duniani. Kwa mfano badala ya kusafiri kutoka Tanzania kwenda Dubai na fedha taslimu jambo ambalo ni hatari, mmiliki atabeba tu kadi yake hadi Dubai na kufanya malipo yake kielektroniki.
- Mastercard inamrahisishia mfanyabiashara kufanya biashara yake hususani swala la malipo. Badala ya kutumia muda mrefu kuhesabu fedha za malipo kutoka kwa wateja au kusubiria mteja aandike hundi, mteja hulipia kwa haraka zaidi kielektroniki na kadi yake ya mastercard.
- Mastercard huongeza mauzo kwa wafanyabiashara kutokana na kwamba, wateja hawaji na fedha kamili mkononi, na uwepo wa mashine inayokubali kadi hizi utamsaidia mfanyabiashara kuwa na wateja waaminifu na wa kudumu.
- Sio rahisi kwa mteja na mfanyabiashara kuibiwa fedha kwa sababu mfumo mzima hufanyika kielektroniki hivyo hakuna pande inayotoa au kupokea fedha taslimu kwa mkono. Vilevile ikiwa kuna makosa yamefanyika ni rahisi kutatua makosa hayo kwa kupiga simu katika taasisi ya kifedha husika ili kupata msaada.
- Kupitia kadi hizi mfanyabiashara huwa na uhakika wa kuuza bidhaa zake kutoka kwa wateja wa nchi mbalimbali. Hivyo ikiwa mteja amefurahishwa na huduma au bidhaa za mteja husika basi ni rahisi kwa mteja huyo kusambaza sifa kuhusu bidhaa au huduma husika hivyo kuwahamasisha wateja wengine kutoka maeneo mbalimbali duniani kutumia au kununua bidhaa au huduma husika.
- Kwa mteja, Ni rahisi kujua taarifa kuhusu matumizi yako ya mwezi, kwa mfanyabiashara ni rahisi kujua taarifa kuhusu mapato yako ya kifedha hivyo ni rahisi kujua kama umepata faida au hasara au kama umetumia fedha nje ya bajeti na nini kifanyike.
- Kwa wanunuzi wa bidhaa mtandaoni, ni rahisi kufanya malipo kupitia Mastercard.
Baadhi ya taasisi zinazotoa kadi za mastercard ni pamoja na CRDB, NMB, NBC, Exim, Standard Chartered, BancABC kupitia mtandao wa simu wa Vodacom na nyingine nyingi.