Home BENKI Serikali kuendelea kuziwezesha benki za kijamii

Serikali kuendelea kuziwezesha benki za kijamii

0 comment 306 views

Serikali imeeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kimfumo ili kuziwezesha benki za biashara na za kijamii (Community Banks) kukua na kushamiri, ikiwemo Benki ya Mucoba.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha Hamad Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuzisaidia Benki za kijamii kama MUCOBA BANK iliyopo mkoani Iringa ili kukuza uchumi wa wananchi wa hali ya chini.

Chande amesema kuwa Hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kutafuta mwekezaji mpya wa MUCOBA, ambaye ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kurekebisha kanuni za usajili wa wakala wa benki kwa kuondoa kigezo cha uzoefu wa miezi 18.

Amezitaja hatua nyingine kuwa ni kuanzisha mfuko maalum wa shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka, kutoa unafuu wa kiasi cha amana ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu (SMR) kwa benki zinazotoa mikopo kwa sekta ya kilimo.

Amebainisha kuwa BoT imepunguza kiwango cha riba kinachotolewa katika akaunti za wateja wa watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi (MNOs) kuwa sawa na riba za amana za sekta ya benki na kudhibiti uwiano wa gharama za uendeshaji wa benki na pato la benki usizidi asilimia 55 na mikopo chechefu isizidi asilimia tano ya mikopo yote.

Akijibu swali la nyongeza kuhusu Benki hiyo kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuchukua fedha zaidi ya milioni 600 kwenye Benki hiyo kupitia Benki ya NMB kwa kisingizio cha Kodi amesema kuwa Fedha hazikuchukuliwa kwa kisingizio cha Kodi bali ilikuwa ni kodi halali.

Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba

Dkt. Nchemba amesema kuwa TRA imeridhia kukutana na Benki hiyo ili kuona namna bora ya kuwasaidia ili benki iweze kujiendesha na kutoa huduma, hivyo amemuomba Mbunge wa Iringa Mjini kuwataarifu viongozi wa Benki hiyo kuonana na uongozi wa juu wa Ofisi TRA ili kutatua changamoto hiyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter