Home BENKI Wauza Bidhaa nje ya nchi wahimizwa kuzingatia sheria

Wauza Bidhaa nje ya nchi wahimizwa kuzingatia sheria

0 comment 297 views

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amewahimiza wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya mipaka ya Tanzania kuzingatia Kanuni za Fedha za Kigeni katika kufanya biashara zao ili kuepuka uuzaji na utumiaji holela wa fedha hizo.

Ameyasema Aprili 5, 2024 wakati akizungumza na wafanyabiashara katika Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.

Gavana Tutuba amesema “kanuni za fedha za kigeni za mwaka 2022 zinamtaka muuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kuhakikisha fedha zitokanazo na mauzo hayo zinawekwa kwenye akaunti zao za benki hapa nchini ndani ya siku 90.

Hata hivyo, tumegundua kwamba baadhi wa wauzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi (exporters) hawatimizi takwa hili la kisheria”.
Ameongeza kuwa BoT imebaini uuzaji holela wa fedha za kigeni miongoni mwa wafanyabiashara hao na amezitaka benki kusitisha huduma kwa wateja wasiotimiza matakwa haya ya kisheria.

Aidha, Gavana Tutuba amesema kurejeshwa kwa Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS)na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs-CGS) unalenga kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kutengeneza mazingira mazuri na wezeshi kwa washiriki wa sekta hiyo ambao aliwataja kuwa wadau muhimu katika kutunisha akiba ya fedha za kigeni.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TCNBC), Dkt. Godwill Wanga ameipongeza Benki Kuu kwa hatua mbalimbali ilizochukua katika kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni na uchumi kiujumla kupitia kuanza kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba ya Benki Kuu.

Ameongeza kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali na Benki Kuu zimefanya upungufu wa fedha za kigeni uliopo nchini kuwa himilivu ukilinganisha na hali iliyopo katika nchi nyingine ulimwenguni.

Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo, wameipongeza BoT kwa mchango wake katika kustawisha sekta ya fedha nchini na wameahidi kushirikiana na BoT katika kutoa elimu ya uuzaji holela wa fedha za kigeni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter