Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kusimamia kwa umakini zoezi la ugawaji vitambulisho kwa wafanyabiashara ili kuwafikia walengwa. Dk. Kebwe amesema hayo katika uzinduzi wa kugawa vitambulisho hivyo na kusisitiza kuwa viongozi hao wa wilaya ndio wasimamizi katika maeneo yao na kuagiza vitambulisho hivyo kutolewa kwa uwazi huku fedha zitakazopatikana baada ya wafanyabiashara kuvichukua zikidhibitiwa kwenda mifukoni mwa watu binafsi.
“Msimamie kwa mujibu wa maelekezo na taratibu zilizopo ili kuongeza mapato ya mkoa wetu kwa kuwa tumeonekana kushuka ikilinganishwa na mwaka 2017. Mkoa umepatiwa vitambulisho 25,000 na vikiuzwa vyote tutapata Sh. 500 milioni, hii itatupandisha zaidi”. Amesema Mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo kutoka manispaa ya Morogoro, Faustin Francis amesema wapo tayari kuchangia pato la taifa kwani hapo awali wameshindwa kufanya hivyo kutokana na kusumbuliwa na mgambo.
“Natoa angalizo kwa wafanyabiashara wakubwa wasitumie mwanya wowote kwa sababu vitambulisho hivi ni vya wafanyabiashara wadogo, kwa sasa tunaanza kutambuana sisi wenyewe”. Amesema