Home KILIMOKILIMO BIASHARA Mahindi ya Tanzania yenye thamani ya Dola milioni 22 kununuliwa na WFP

Mahindi ya Tanzania yenye thamani ya Dola milioni 22 kununuliwa na WFP

0 comment 75 views

Shirika la Chakula Duniani (WFP) limepanga kununua tani 60,000 za mahindi meupe yenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 22.

WFP linatarajia kununua mahindi hayo kutoka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa Randama ya Mashirikiano kati ya CPB, NFRA na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Juni 05, 2024, jijini Dodoma, Mwakilishi Mkazi wa WFP Sarah Gordon-Gibson amesema wana ushirikiano wa kihistoria na Tanzania katika kuhakikisha usalama wa chakula, lishe na soko la mazao kwa wakulima wadogo.

Gordon-Gibson amefafanua kuwa, Mwaka 2009 WFP na NFRA zilifanya kazi pamoja kuwawezesha wakulima wadogo na kuchochea masoko ya ndani kupitia ununuzi wa mazao huku ukiwapa kipaumbele maalum wakulima wadogo.

“Kuanzia mwaka 2011 hadi 2023, WFP imenunua kutoka NFRA zaidi ya tani 223,000 za mahindi meupe na karibu tani 4,000 za mtama zenye thamani ya jumla ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 60.

Mwaka 2024, WFP inapanga kununua tani 60,000 za mahindi meupe kutoka NFRA na CPB kwa jumla ya thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 22, ambapo WFP imekuwa ikikodisha maghala ya NFRA mjini Dodoma kuanzia mwaka 2011 hadi 2023 kwa Dola za Marekani 213,000”, amesema Gordon-Gibson.

Ameongeza kuwa, kuanzia mwaka 2017 hadi Mei 2024, WFP ilinunua tani 54,000 za mahindi, maharage na mtama zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 15 kutoka CPB.

Aidha, WFP imekuwa ikikodi vifaa vya ghala vya CPB kwa Dola za Marekani 96,000 na kushirikiana katika huduma ya kusaga mahindi iliyoimarishwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa kwa gharama ya Dola za Marekani 84,000.

“Shirika litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula, lishe na soko la mazao nchini,” amesema Gordon-Gibson.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameshiriki katika hafla hiyo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Kilimo na WFP.

Viongozi waliohudhuria ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo akiwemo Makamu Mwenyekiti Mariam Ditopile.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter