Home FEDHA Uchumi wa Tanzania Bara, Zanzibar unazidi kuimarika: BoT

Uchumi wa Tanzania Bara, Zanzibar unazidi kuimarika: BoT

0 comment 12 views

Mwenendo wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuwa imara mwaka 2024 na mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu katika kipindi chote cha mwaka 2024, ukiwa chini ya lengo la asilimia 5 kwa Tanzania Bara kwa wastani wa asilimia 3 na kwa Zanzibar mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.5 mwezi Novemba 2024.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba ameeleza hayo wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu mbele ya wakuu wa benki na taasisi za fedha na waandishi wa habari, Januari 08, 2025.

“Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia 4 kutokana na kuendelea kuwepo kwa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, yakiwemo mafuta ghafi, amesema Gavana Tutuba.

Gavana Tutuba amesema ukuaji wa ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9.

Ukwasi wa fedha za kigeni uliongezeka kwa kiwango kikubwa katika robo ya nne ya mwaka 2024.  Hali hii inatokana na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha duniani kutokana na kupungua kwa riba katika nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni nchini kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku.

Ameongeza kuwa kutokana na kuimarika kwa ukwasi wa fedha za kigeni nchini, shilingi iliimarika dhidi ya fedha za kigeni, soko la fedha za kigeni lisilo rasmi lilitoweka, na matarajio kuwa thamani ya shilingi itaendelea kushuka yalififia, hali ambayo imekuwa na manufaa ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo, na kupunguza gharama ya kulipa madeni nje ya nchi.

Thamani ya shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, kutokana na kuwepo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024 kutokana na utekelezaji wa sera ya fedha na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter