Katika kuhamasisha matumizi ya mashine za kielektroniki nchini, serikali inatarajia kufungua Tuzo ya Uzalendo ambapo wananchi wataweza kujipatia zawadi kupitia risiti za kielektroniki.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Robert Manyama, wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika Mkoani Kigoma.
“Serikali ina jukumu kubwa la kuweka mikakati ya kuendelea kurasimisha biashara nchini na kuhamasisha utumiaji wa mashine za kielektroniki katika utoaji wa risiti ikiwa ni pamoja na kutumia risiti hizo kujipatia zawadi kupitia Tuzo ya Uzalendo inayotarajiwa kufunguliwa rasmi hivi punde,’ ameeleza Manyama.
Manyama amesema, maoni mbalimbali yanayotolewa katika Makongamano hayo ya Kodi yatasaidia kuibua vyanzo vipya vya mapato na kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje pamoja na kuendelea kubainisha maeneo yenye changamoto zaidi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo – TCCIA Mkoa wa Kigoma Obadi Kabuga amesema kuwa Kongamano hilo la Kodi limekuwa funzo na litasaidia Serikali kufanya biashara kwa kushirikiana na nchi zinazoizunguka, kwani sera zilizopo zinakinzana na sera za nchi jirani na kuiomba Serikali kufanya utafiti wa sera zake kabla ya kupeleka maboresho ya sera katika Bunge lijalo 2025/2026.
“Tunaomba mabadiliko ya Sera yatakapopelekwa Bungeni yafanyiwe utafiti kabla ya kufanya mabadiliko. Wenzetu wana sera gani, ili zitakapokuja zile sera jumuishi ambazo zitakuwa na mfanano zitaleta uchumi mzuri na hususan katika Mkoa wetu wa Kigoma pamoja na Tanzania nzima” amefafanua Kabuga.
Kabuga amehitimisha kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiamini TCCIA pamoja na Wizara ya Fedha kwa pamoja kuandaa Makongamano hayo ya Kodi Kikanda, ambapo mwitikio kwa wanakigoma ulikuwa mkubwa na wameitumia fursa hiyo vizuri kwa kutoa maoni na changamoto mbalimbali.
Kongamano hili la Kodi bado liko kwenye Kanda ya Ziwa (Kigoma). Makongamano haya ya Kikanda yalianzia Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Kaskazini Arusha na yanaendelea katika Kanda nyingine.