Na Mwandishi wetu
Kampuni ya Alaf ambayo inajihusisha na kutengeneza mabati hivi karibuni imeanzisha kiwanda jijini Mwanza lengo likiwa ni utekelezaji wa sera ya viwanda hapa nchini. Kiwanda hicho kimeanzishwa kutokana nyumba nyingi katika kanda ya ziwa bado huezekwa kwa nyasi hivyo wawekezaji wameona ni fursa nzuri kuanzisha kiwanda cha mabati kwani soko ni la uhakika.
Katika ufunguzi wa kiwanda hicho ambacho kimejengwa katika Kata ya Igogo, Kiongozi wa mbio za mwenge Amour Hamad Amour amepongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kuona fursa ya soko na kuitumia. Amewakaribisha wawekezaji zaidi kuja Mwanza kuwekeza.
Mbali na hayo, Amour amewataka wananchi wa Mwanza kuchangamkia fursa kama hizi ili kuongeza soko la ajira kwa vijana. Ameshauri viongozi wa wilaya na halmashauri ya Mwanza kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Mwanza ilikuwa na nyumba za kaya 481,107 na asilimia 25.3 ya nyumba hizo zilikuwa zimeezekwa na nyasi.