Home VIWANDA Tanzania, Misri kujenga kiwanda cha kuchakata nyama

Tanzania, Misri kujenga kiwanda cha kuchakata nyama

0 comment 138 views

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Misri inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha uchakataji nyama mkoani Pwani ambapo imeelezwa kuwa Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) na Kampuni ya Uwekezaji ya Misri (Necai) ndio waratibu. Hadi sasa, makubaliano ya awali ya ujenzi tayari yamesainiwa kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Narco, Prof. Philemon Wambura pamoja na Ofisa wa bodi ya kampuni ya Necai, Jenerali Ahmed Hassan.

Akizungumza wakati wa kuweka saini makubaliano hayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema anatarajia kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa kwani takribani asilimia 1.4 ya mifugo yote inatoka hapa nchini huku asilimia 11 ya mifugo barani Afrika ikipatikana nchini Tanzania.

“Tanzania ina mikataba mbalimbali ikiwemo ya uhifadhi na utunzaji wa mifugo, huku Wizara ikiwa bega kwa bega na wafugaji ili kuzalisha mifugo bora na kuwa na nyama shindani pamoja na kuwa na mbari bora za mifugo. Kupitia ujenzi huo, utasaidia kuendelea kukuza uchumi na kutakuwa na soko kubwa nchini Misri, Afrika na dunia kwa ujumla”. Amesema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Misri nchini Tanzania ambaye pia alihudhuria utiaji saini makubaliano hayo, amesema ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili umefanikisha hatua hiyo ya ujenzi wa kiwanda na kuongeza kuwa nchi zote mbili zitanufaika.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mradi huo utajikita zaidi kwenye kuchakata nyama na kuiongezea thamani na vilevile kuongeza thamani ngozi na bidhaa zake.

“Ujenzi utaleta mapinduzi makubwa sekta ya mifugo, ambapo ng’ombe ataingia kiwandani akiwa hai, lakini akitolewa nyama ambayo itaweza kuuzwa nchini na nje ya nchi na ngozi ikiwa imeongezewa thamani”. Amesema Ulega.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter